Rasimu ya Katiba imetolewa na Tume ya marekebisho ya katiba na miongoni
mwa mambo yanayopendekezwa ni kuundwa kwa Serikali tatu pamoja na
kuruhusiwa kwa mgombea binafsi.
Uzinduzi
wa rasimu hiyo ya katiba umefanyika jana, Dar es Salaam na kwa uamuzi
huo wa tume sasa Tanzania itakuwa na marais watatu ambao ni rais wa
serikali ya shirikisho, rais wa Tanzania Bara na rais wa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Alisema tume yake inapendekeza serikali
tatu, kwani wananchi ambao walitoa mapendekezo hayo ni wengi kuliko
makundi ya waliotaka serikali moja, serikali nne, muungano wa mkataba na
serikali mbili.
"Sababu
zao zilikuwa nzito lakini pia kulikuwa na changamoto nyingi na nzito.
Pamoja na maoni ya wananchi, tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo
huu zilizotolewa na tume zilizopita na tafiti zilizofanywa na tume
kuhusu aina mbalimbali za muungano," alisema Warioba.
Alisema
pamoja na maoni ya wananchi, tume ilirejea sababu za kupendekeza muundo
huo zilizotolewa na tume zilizopita na tafiti zilizofanywa na tume
kuhusu aina mbalimbali za muungano.
"Baada
ya yote hayo tume hatukuwa na jinsi zaidi ya kufikia uamuzi wa
kupendekeza mfumo wa serikali tatu, yaani serikali ya shirikisho,
serikali ya Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar," alisema
Warioba.
Hivyo
kutakuwa na serikali ya muungano, serikali ya Tanzania Bara, Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar. Shughuli za Muungano zitatekelezwa na
kusimamiwa na serikali ya muungano, Bunge la Jamhuri ya Muungano na
mahakama yake.
Kutokana na uamuzi huo wa tume, muundo, madaraka na
mambo mengine ya kiuendaji yahusuyo serikali ya Bara na ile ya Zanzibar
yataainishwa katika katiba za washirika hao wa muungano.
Katika
rasimu hiyo serikali ya muungano itakuwa ndio chombo chenye mamlaka ya
utendaji, Bunge litakuwa na mamlaka ya kutunga sheria kwa mambo ya
muungano na mahakama kitakuwa chombo cha kutoa haki katika muungano huo.
Kwa
mujibu wa rasimu hiyo, serikali ya Bara itakuwa na mamlaka juu ya mambo
yasiyo ya muungano yanayohusu eneo hilo na SMZ, pia itakuwa na mamlaka
ya juu yasiyo ya muungano yaliyoko eneo lake. “Washirika wa muungano
watakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya muungano na watatekeleza."
Washirika
hao wanaruhusiwa kuanzisha mahusiano au ushirikiano na jumuiya au
taasisi yoyote ya kikanda au kimataifa kwa mambo yaliyo chini yake kwa
mujibu wa katiba yake.
Katika
eneo hilo inapendekezwa kuwa mshirika wa muungano anaweza wakati wa
kutekeleza majukumu yake kuomba ushirikiano kutoka serikali ya muungano
kwa ajili ya kufanikisha uhusiano na jumuiya au taasisi za kimataifa au
kikanda na serikali ya muungano inaweza kutoa ushirikiano kwa mshirika
huyo kwa namna itakavyohitajika.
Inapendekezwa kila mshirika wa
muungano atateua waziri mkazi atakayeratibu na kusimamia uhusiano baina
ya serikali za washirika na kati ya serikali ya mshirika na serikali
ya muungano, mawaziri hao wakaazi watafanya kazi zao na ofisi zao
zitakuwa makao makuu ya serikali ya muungano na watakuwa kiungo kati ya
serikali ya muungano na serikali mshirika
Tume
hiyo pia imepunguza mambo ya muungano kutoka 22 hadi saba ambayo ni
katiba na mamlaka ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama
wa Jamhuri, uraia na uhamiaji, sarafu na benki kuu, mambo ya nje,
usajili wa vyama vya siasa, ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi
yatokanayo na mambo ya muungano.
Katika
muundo huo serikali ya muungano itapata mamlaka yake kutoka kwa
wananchi wa pande zote na serikali za serikali washirika nazo
zitachaguliwa na wananchi kupitia uchaguzi wa kidemokrasia
utakaosimamiwa na tume za uchaguzi za nchi zao. Viongozi wote hao
wanalazimishwa na katiba hiyo kulinda na kuimarisha muungano.
Jaji
Joseph Warioba alisema tume yake imezingatia maoni ya wananchi ambao
walipendekeza haki zote ziimarishwe na kusiwe na vikwazo vya lazima.
Kutokana
na maoni hayo, Warioba alisema tume yake inapendekeza kwamba vikwazo
vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe, kwa maana nyingine tume
inapendekeza mgombea binafsi aruhusiwe.
Kwenye
rasimu hiyo ya katiba, pia haki mpya zimeingizwa ambazo ni haki ya
mtoto, haki za watu wenye ulemavu, haki za wanawake, haki za wazee, haki
za makundi madogo katika jamii, haki ya elimu na kujifunza, haki ya
kupata habari, haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari.
Rais
wa shirikisho ndiye atakayekuwa amiri jeshi mkuu na yeye atakuwa na
makamu mmoja. Rais huyo atakuwa ndiye taswira ya Muungano wa Tanzania.
Pia kutakuwa na bunge la muungano, na mahakama ya Muungano.
Makamu wa Rais ndiye atakayekuwa msaidizi mkuu wa Rais.
Tume
hiyo imependekeza umri wa kugombea urais uendelee kuwa miaka 40 kwa
vile idadi kubwa ya watu waliotoa maoni walipendekeza umri huo.
Kwenye
mapendekezo hayo, Warioba alisema mgombea wa nafasi ya rais atatangazwa
kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya asilimia 50 ya kura
zote zilizopigwa.
Inapendekezwa kuwa uchaguzi wa rais itakuwa kama
ilivyo sasa isipokuwa tume hiyo imependekeza mgombea urais aweza
kupendekezwa na chama cha siasa au kuwa mgombea huru.
Katika
rasimu hiyo tume hiyo imependekeza kuwa matokeo ya uchaguzi wa Rais
yanaweza kulalamikiwa mahakamani. 'lakini sio kila mtu anaweza kufungua
kesi, wanaoweza kufungua kesi ni wagombea urais.'
Pia
tume hiyo imependekezwa kuundwa kwa mahakama ya juu (supreme court)
ambako wagombea urais wanaweza kufungua kesi na ni mahakama hiyo tu
itakuwa na mamlaka na uwezo wa kusikiliza malalamiko kuhusu matokeo ya
uchaguzi wa rais na shauri lazima liamuliwe ndani ya siku thelathini.
"Rais aliyeshinda ataapishwa siku 30 tangu alipotangazwa kuwa mshindi au kuthibitishwa na mahakama," alisema Warioba.
Warioba
alisema katika eneo hilo tume imependekeza rais abaki na madaraka ya
uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu. Lakini imependekezwa rais
ashirikiane na taasisi na vyombo vingine katika uteuzi huo.
Alisema
uteuzi wa mawaziri na manaibu waziri Rais atateua na Bunge
lithibitishe, lakini kuhusu jaji mkuu na naibu jaji mkuu ambaye tume
imependekeza cheo hicho kiwepo, majina ya watu waliopendekezwa na tume
ya utumishi wa mahakama na baada ya hao bunge litathibitisha. Kwa upande
wa makatibu wakuu watateuliwa na rais kutokana na mapendekezo ya tume
ya utumishi wa umma.
Kwa
upande wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, inapendekezwa kuwa
kianzishwe chombo kipya kitakachoitwa baraza la ulinzi na usalama wa
taifa ambalo kati ya majukumu yake itakuwa ni kumshauri rais kuhusu
uteuzi wa wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Kinga ya rais imependekezwa na tume hiyo ibaki na anaweza kushtakiwa na Bunge kama ilivyo katiba ya sasa.
Katika
mapendekezo hayo imependekezwa kuwa rais aunde serikali ndogo iliyo na
mawaziri wasiozidi 15 na mawaziri hao wasiwe wabunge. Mawaziri hao
hawatahudhuria vikao vya Bunge isipokuwa watahitajika kutoa ufafanuzi
kwenye kamati za Bunge.
Kwa
upande wa Bunge, Warioba alisema inapendekezwa wabunge wa aina mbili.
Yaani kutakuwa na wabunge wa kuchaguliwa na wabunge wachache wa
kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu. Tume imependekeza
mbunge akifukuzwa na chama cha siasa abaki kuwa mbunge lakini akihama
chama atapoteza ubunge wake.
Katika
eneo hilo pia rasimu inapendekeza kuwepo ukomo wa ubunge ambao ni
vipindi vitatu vya miaka mitano mitano lakini wananchi wanaweza
kumwondoa mbunge wao kabla ya mwisho wa kipindi iwapo hawaridhiki na
utendaji wake wa kazi.
Pia
imependekezwa kusiwepo na uchaguzi mdogo isipokuwa kama nafasi
inayokuwa wazi inatokana na mbunge huru ndipo uchaguzi mdogo kujaza
nafasi hiyo utafanyika, "lakini kama nafasi ikiwa wazi kutokana na
mbunge wa chama cha siasa basi nafasi hiyo ijazwe na mtu kutoka chama
hicho.”
Kwa upande wa spika na naibu spika, inapendekezwa wasitokane na wabunge na wasiwe viongozi wa vyama vya siasa.
Jaji
Warioba alisema tume yake imefanya uchambuzi wa maoni ya wananchi
katika eneo hilo na imependekeza jina la tume liwe Tume Huru ya
Uchaguzi. Tume pia imependekeza sifa za wajumbe wa tume hiyo huru
ziwekwe kwenye katiba na watapatikana kutokana miongoni mwa watu wenye
sifa zilizoainishwa ndani ya katiba kwa kuomba.
Alisema
majina ya waombaji yatachambuliwa na kamati ya uteuzi ambayo mwenyekiti
wake atakuwa jaji mkuu na wajumbe wengine sita ambao ni majaji wakuu wa
nchi washirika, spika wa bunge la Jamhuri ya Muungano na maspika wa
mabunge ya nchi washirika na mwenyekiti wa tume ya haki za binadamu.
Alisema
kamati hiyo itapendekeza majina ya watu wnaofaa kwa rais ambaye atateua
mwenyekiti, makamu mwenyekiti na wajumbe wengine.
"Bunge
litathibitisha uteuzi wao, wabunge na viongozi wengine wa kisiasa
hawatakuwa na sifa za kuwa wajumbe wa tume ya uchaguzi."
Katika
eneo hilo imependekezwa kuwa tume huru ya uchaguzi isimamie masuala ya
uchaguzi, kura ya maoni na usajili wa vyama vya siasa.
Kuhusu
mahakama imependekezwa kuwa majaji wa mahakama ya juu (supreme court)
na mahakama ya rufaa watateuliwa na rais baada ya kupendekezwa na tume
ya utumishi wa mahakama.
Kwa
kuwa tume imependekea muungano wa shirikisho, kutokana na uzito wa
maoni ya wananchi, hivyo kutakuwa na benki kuu ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania itakayokuwa na wajibu wa kusimamia masuala ya sarafu na fedha
za kigeni na benki za washirika wa muungano.
Pia
inapendekezwa kuwepo na benki zitakazokuwa na jukumu la kutunza akaunti
ya fedha za serikali za kila mshirika wa Muungano na kuzisimamia benki
za biashara katika mamlaka zao.
Katiba inapendekeza makamu wa rais atatoka upande mwingine wa muungano ambako hatoki rais wa muungano.
Mgombea
binafsi anaruhusiwa kumteua makamu wa rais hata kama mtu huyo
alishashika wadhifa wa urais wa Zanzibar au wa Tanzania bara. Ikitokea
rais wa bara au wa SMZ akateuliwa kuwa makamu wa rais atalazimika kuacha
wadhifa wake wa awali ili ashike wadhifa huo wa juu katika Jamhuri.
Kwa
muundo huo baraza la mawaziri sasa litaundwa na makamu wa rais wa
Jamhuri ya muungano, mawaziri wa serikali ya muungano, mwanasheria mkuu
wa serikali atahudhuria vikao vya baraza hilo lakini hatakuwa na haki ya
kupiga kura.
Baraza hilo la mawaziri ndilo litamshauri rais na bunge
na mahakama havitakuwa na uwezo wa kuchunguza jambo ambalo limepitishwa
na baraza la mawaziri.
Katiba
iliyopendekezwa ina ibara 20 kutoka za sasa ambazo ni 153. Misingi
mikuu ya taifa iliyoko kwenye katiba hiyo ni saba kutoka minne ya awali
ambayo ni uhuru, haki, udugu, usawa, umoja, amani na mshikamano.
Tunu za taifa katika katiba hiyo ni utu, uzalendo, uadilifu, umoja, uwazi, uwajibikaji, na kiswahili.
Kwenye
katiba hiyo pia kuna malengo ya taifa ambayo yatakuwa ni mwongozo kwa
serikali, bunge, mahakama, vyama vya siasa, taasisi na mamlaka nyingine
kwa kila mwananchi katika matumizi au kutafsiri masharti ya katiba au
sheria nyingine za nchi.
Kwa msingi huo, tume hiyo imependekeza
malengo makuu ya taifa yapanuliwe kwa mpango wa kuonyesha malengo ya
kisiasa, kiuchumi, kijamii, kiutumaduni, kimazingira, na sera ya mambo
ya nje.
Vyombo
vya kikatiba katika rasimu hiyo ni tume ya uhusiano na uratibu wa
serikali, baraza la mawaziri, kamati maalum ya makatibu wakuu na
sekretarieti ya baraza la mawaziri, baraza la ulinzi na usalama la
taifa, tume huru ya uchaguzi, tume ya utumishi wa mahakama, tume ya
utumishi wa umma, tume ya maadili ya viongozi na uwajibikaji na tume ya
haki za binadamu na utawala bora.
Katika
katiba hiyo inapendekezwa kuwa maadili ya viongozi wa umma pamoja na
miiko ya uongozi yawekwe kwenye katiba na tume imependekeza sekretarieti
ya maadili ibadilishwe kuw atume yenye mamlaka makubwa ya kusimamia
maadili ya viongozi wanaovunja miiko ya uongozi.