
MBUNGE wa Karagwe, Gosbert Blandes (CCM), amehoji lini serikali itapitisha Kiswahili kitumike kuanzia Shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu. Aidha, alisema mwaka 2004, Umoja wa Afrika ulipitisha Kiswahili kiwe ni lugha ambayo itatumika katika mikutano na shughuli mbalimbali.
“Je, serikali imejiandaa vipi kupeleka wakalimani wa kutosha kutoka Tanzania ili waweze kujipatia ajira?” alihoji.
Akijibu
 maswali hayo, Naibu Waziri wa  Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, 
Amos Makala alisema jitihada  zinafanywa na taasisi hizo za kukuza 
Kiswahili mojawapo kuandika vitabu  vingi vya kufundishia na kuongeza 
wataalamu.
“Nasema
 wazo hilo tumelipokea na sisi  ndani ya serikali tunaendelea kulifanyia
 kazi na hata wakati  tunawasilisha bajeti yetu zilitoka hoja hizo za 
kuwa Kiswahili  kifundishwe madarasani,” alisema.
Aidha, Makala alikiri kupitishwa kwa azimio hilo na kuongeza kuwa:
“Kama
 Tanzania tumeona kuwa hii ni fursa  muhimu na tayari moja ya kazi 
zinazofanywa na Taasisi za kukuza  Kiswahili, BAKITA, BAKIZA ni kuongeza
 wataalamu zaidi ili waweze kupata  ajira hiyo.”
Aliongeza
 kuwa Tanzania kama Tanzania  mjini Addis Ababa kuna kituo cha 
kufundishia lugha ya Kiswahili. Awali  katika swali la msingi, Mbunge wa
 Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM)  alitaka kufahamu kama nchini Tanzania
 kuna Sera ya Lugha.
Pia, alihoji kama ipo, je, sera hiyo ya Lugha imeipatia hadhi gani lugha ya Kiswahili.
Aidha,
 alitaka kujua kuna mkakati gani  mahsusi wa kuifanya Lugha ya Kiswahili
 kuwa ya kufundishia kwa viwango  vyote vya elimu hapa nchini.
Akijibu
 swali hilo, Makala alisema  Tanzania hakuna andiko mahususi au 
linalosimama pekee kama Sera ya  Lugha, bali suala la lugha 
limezingatiwa kama Sura maalumu muhimu ndani  ya Sera ya Utamaduni ya 
mwaka 1997.
Alisema
 katika andiko hilo la sera ya  Utamaduni, Kiswahili kimetambuliwa kuwa 
siyo tu lugha ya mawasiliano  mapana nchini bali pia ni lugha ya taifa 
na mojawapo ya lugha rasmi  mbili za Taifa.
Aidha,
 alisema miongoni mwa mikakati  mahsusi ya kuifanya lugha ya Kiswahili 
kuwa lugha ya kufundishia ni  jitihada zinazoendelea za wataalamu wa 
Asasi za ukuzaji wa Kiswahili  nchini ambazo ni kuboresha sarufi ya 
Kiswahili, kutunga Kamusi za  Kiswahili za masomo na taaluma mbalimbali.