Ssenkoom kushoto akizungumza na mwandishi Uwanja wa Ndege Dar es Salaam jana usiku |
BEKI mpya wa Simba SC, Robert Ssenkoom amesema kwamba anataka kuitumia klabu hiyo kama daraja la kupandia kwenda Ulaya kucheza soka ya kulipwa.
Akizungumza na mwandishi baada ya kuwasili Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam usiku wa jana, Ssenkoom anayetokea URA ya kwao, Uganda alisema kwamba kiu yake ni kucheza Ulaya.
Beki huyo mwenye mwili sawa na beki mwingine aliyehama Simba kujiunga na watani wa jadi, Yanga SC msimu huu, Kevin Yondan, alisema anaamini timu yake mpya itamsaidia kutimiza ndoto zake hizo.
“Ina mashabiki wazuri, wanajua kuwasapoti wachezaji wao. Nataka niwe beki bora hapa Tanzania, nina matumaini ya kufanya vizuri na ninawaahidi mambo mazuri tu wapenzi wa Simba SC,”alisema.
Ssenkoom ambaye amesaini Mkataba wa miaka miwili Simba SC amesema wapenzi wa klabu hiyo watarajie kumuona anaanza mazoezi mara tu atakapokabidhiwa vifaa vya mazoezi.
Beki huyo alitua majira ya saa 6 usiku wa jana Dar es Salaam na kulakiwa na viongozi na wapenzi wachache wa timu hiyo.
Anakuwa Mganda wa tatu katika kikosi cha Simba, baada ya kipa Abbel Dhaira na kiungo Mussa Mudde na kama Wekundu hao wa Msimbazi watafanikiwa kumsajili Moses Oloya basi atakuwa anacheza timu moja ndugu zake watatu.
Kocha Msaidizi wa Simba SC, Moses Basena pia anatokea Uganda na ndiye aliyefanikisha usajili wa beki huyo na anashughulikia pia mipango ya Oloya kutua Msimbazi.
Simba SC imekuwa ikihaha kuimarisha safu yake ya ulinzi tangu impoteze beki Kevin Yondan aliyenyakuliwa na watani, Yanga SC.
Mwanzoni mwa msimu ilimsajili Lino Masombo kutoka DRC, ikamtema, baadaye ikamsajili Mbuyu Twite kutoka Rwanda, lakini Yanga pia wakaingilia na kumbadili mawazo akageuza njia kwenda Jangwani alipo sasa.
Ikamsajili Paschal Ochieng kutoka Kenya, lakini haikuridhika naye ikamtema. Ikamsajili Komabil Keita naye pia haikuridhika naye ikamtema na katika mechi za mwishoni za msimu ikalazimika kuwapanga pamoja katika beki ya kati, Shomary Kapombe na Mudde, ambao kidogo walipunguza matatizo.
Baada ya kutua kwa Ssenkoom, sasa kocha mpya wa Simba SC, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ atakuwa na jukumu la kumtafutia mtu sahihi wa kucheza naye pale katikati, kama atakuwa Kapombe ama Mudde au yeyote, ili mradi kutengeneza ukuta imara.