KLABU ya Manchester City imemuorodhesha kiungo mwenye kasi wa Atletico Madrid, Olivier Torres katika orodha ya wachezaji inayowataka kuwasajili mwishoni mwa msimu.
Msaka vipaji wa klabu hiyo, David Fernandez alimshuhudia kinda huyo wa miaka 18 akiingia dakika ya 72 kutokea benchi, Atletico ikitoka sare ya bila kufungana na Deportivo La Coruna.
Ni huyu: Torres anayetakiwa na Manchester City
Torres, anayechezea timu ya taifa ya vijana ya Hispania chini ya umri wa miaka 21, ana thamani ya Pauni Milioni 8 na klabu za Manchester United, Chelsea na Liverpool pia zimekuwa zikimfuatilia.
City pia imeonyesha nia ya kuwasajili beki wa kulia Velez Sarsfield na Gino Peruzzi. Kinda huyo wa miaka 20 wa Argentina, ambaye pia anaweza kucheza nafasi ya winga, aliwavutia wasaka vipaji mwaka jana katika michuano ya Copa Libertadores. Inter Milan pia inamtaka.