Wednesday, 1 May 2013

UCHAFU WA KINANA WAANIKWA BUNGENI NA MCH. MSIGWA (MB-IRINGA MJINI)


Kambi ya Upinzani Bungeni imetoa tuhuma nzito kwa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ikidai kuwa anajihusisha na mtandao wa ujangili nchini. Hata hivyo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi amejibu tuhuma hiyo akisema ni za uongo huku akiituhumu kambi hiyo kuwa imedanganya wakati inajua ukweli kuhusu tuhuma dhidi ya Kinana. Akiwasilisha maoni ya upinzani kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka 2013/14, Msemaji wa Kambi ya Upinzani kuhusu Maliasili, Mchungaji Peter Msigwa alisema vitendo vya ujangili vimekuwa vikilitia doa taifa kwenye jumuiya za kimataifa.

“Kwa bahati mbaya ni kwamba wahusika wengi ambao wanatajwa kwa ushahidi ni makada maarufu na wengine ni viongozi waandamizi wa CCM,” alisema Mchungaji Msigwa.

“Tumeshuhudia watuhumiwa wengine wa ujangili ambao Ikulu imediriki kuwapatia nafasi kubwa za uongozi wa taifa hili, licha ya kutajwa kwenye ripoti ya uchunguzi kuhusiana na ujangili.”

Alisema mwaka 2009, meli ya Kampuni ya Wakala wa Meli ya Sharaf Shipping inayomilikiwa na Kinana ilikamatwa China ikiwa na makontena yenye nyara za Serikali ikiyasafirisha kwenda Hong Kong.

“Nyaraka zilizopo Ofisi za Wakala wa Usajili wa Kampuni na Biashara (Brela), zinaonyesha kuwa kampuni hiyo ya Kinana ilisajiliwa Oktoba 2003 na kupewa hati na. 47221.

“Nyaraka zinaonyesha kuwa Kinana anamiliki hisa 7,500 kati ya 10,000 za kampuni hiyo iliyosajiliwa Dar es Salaam. Mshirika mwenzake katika kampuni hiyo, Rahma Hussein ambaye ni mke wake anamiliki hisa 2,500,” alisema Msigwa.