Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano wa Microsoft Africa, Louis Onyango Otieno akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mihayo Wilmore na Mkurugenzi wa Utambuzi COSTECH, Faith Shimba.
DAR ES SALAAM, Tanzania
KAMPUNI za Microsoft na Uhuru One, wameanza mpango wa majaribio wa utoaji wa elimu ya Teknolojia ya Mawasiliano (Tehama) kwa kutumia mkongo wa Taifa kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu lengo likiwa kuibua uvumbuzi mpya katika sekta hiyo.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Masuala ya Sheria na Uhusiano wa Microsoft Africa, Louis Otieno alisema mpango huo utachukua miezi sita hadi mwaka mmoja.
Alisema mpango huo umewalenga wanafunzi kwa kuwa ndio kundi kubwa ambalo linaingia katika shughuli za uzalishaji ikiwa ni pamoja na ajira, ujasiriamali na ukweli kuwa ngazi ya elimu ya juu ndipo ambapo wanafunzi wanakuwa katika hali ya kuweza kubadilika.
"Tumeangalia ngazi ya vyuo kwa kuwa ndio ambapo wanafunzi wanabadilika na hata kuweza kufanya uvumbuzi" alisema na kuongeza kuwa Tanzania ina vipaji vngi ambavyo vimeweza kufanya uvumbuzi katika eneo jingine lakini sio katika Teknohama.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mtendaji wa wadau wa Uhuru One, Mihayo Wilmore alisema mpango huo umelenga watu kuweza kuutumia mkongo wa Taifa katika shughuli za habari na mawasiliano hususan maeneo ya vijijini.
Alisema mkongo wa Taifa umefika hadi katika ngazi ya wilaya lakini lakini umekuwa hautumiki hali ambayo alisema chini ya makubaliano hayo yana lengo la kuhakikisha hali inakuwa tofauti na majaribio yanayofanyika ni endelevu na wadau zaidi wanakaribishwa.