Tuesday, 14 May 2013

MAGUFULI:TUTABOMOA NYUMBA ZA CCM NA CHADEMA BILA KUJALI ILI KUPISHA UJENZI WA BARABARA

 
Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli jana amesema kwamba atabomoa nyumba za wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chadema bila kujali nyumba ni za kina nani na amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa kufanya safari nyingi za nje kwa kuwa anatafuta fedha za ujenzi wa barabara.

Amesema wamekuwa wakipata wakati mgumu wakati wa kutengeneza barabara. " Kuna mti mkandarasi alijaribu kuung'oa kwa magreda kuanzia asubuhi mpaka jioni, lakini tulishindwa mpaka tulipowaomba wazee wa lile eneo, walipokubali, mti ulianguka wenyewe. Kazi ni ngumu sana, msione hivi,"amesema Dk Magufuli.

Dk Magufuli amesema kwamba hatajali wala kuogopa kuvunja nyumba ya mtu yeyote kwa kuwa serikali inafanya hivyo kwa maslahi ya wanachi wote na taifa kwa ujumla.

Mbali na hayo amewashangaa wabunge wa upinzani kwa kutosifia juhudi za ujenzi zinazofanywa na serikali ya CCM. "Katika Jimbo la Mheshimiwa John Mnyika kuna barabara imetengenezwa, lakini sijasikia akiisifia..., wapinzani wanakosoa kila kitu. Lazima mkubali ujenzi wa barabara unapangwa na kusimamiwa na serikali ya CCM, hapo hakuna ubishi," amesema.

Pia amesisitiza kwamba watu wote waliojenga ndani ya hifadhi ya barabara umbali wa mita 22.5 na marekebisho ya sheria ya mwaka 2005 ambayo anayejenga ndani ya hifadhi ya barabara umbali wa mita 30 pia wote watabomolewa kwa kuwa ni kinyume cha sheria.

Wakati akimalizia kuwasilisha hoja yake, Dk Magufuli amesema kwamba wabunge wote wa upinzani na chama tawala wamechangia vizuri mjadala wa wizara yake.

Dk Magufuli amesema hayo wakati akihitimisha Bajeti Wizara ya Ujenzi.


Bunge tayari limeipitisha bajeti hiyo