Saturday, 4 May 2013

BOCCO NA MWANTIKA HALI MBAYA RABAT, HAWAJALA TANGU BAADA YA MECHI

David Mwantika

Na Mahmoud Zubeiry, Rabat
UNAWEZA kuwaonea huruma. Hawana raha na hawajala tangu jana. Wachezaji wawili wa Azam, beki David Mwantika ‘Bedui’ na mshambuliaji John Raphael Bocco ‘Adebayor’ wako katika hali mbaya na kutokana na kusononeka kwa kuchangia kwa kiasi kikubwa timu yao kutolewa na AS FAR Rabat katika Kombe la Shirikisho.   

Azam jana ilifungwa mabao 2-1 na Rabat kwenye kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah na wenyeji AS FAR Rabat na kutolewa katika Raundi ya Tatu ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Mwantika aliidhoofisha Azam jana kwa kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 56 kwa kumchezea rafu mchezaji wa Rabat na pia alisababisha penalti iliyowapa bao la kwanza Rabat dakika ya 12 ambalo lilikuwa la kusawazisha, baada ya Bocco kutangulia kufunga dakika ya sita.

Kwa ujumla, Mwantika jana hakuwa katika ubora wake- kwani hata faulo alizocheza na kusababisha penalti ilikuwa ‘si ya lazima’ na hata kadi nyekundu pia angeweza kuiepuka kama asingemsukuma hadi kwenye lami mchezaji wa Rabat.  
Azam ilihitaji sare yoyote ya mabao ifuzu na ilikaribia kuipata dakika ya 81 ilipopata penalti ikiwa nyuma kwa mabao 2-1, lakini fundi wa upigaji wa michomo hiyo, John Raphael Bocco alikwenda kugongesha mwamba wa juu mpira huo.

Dakika ya 88, kona nzuri iliyochongwa na Khamis Mcha ‘Vialli’ iliunganishwa vizuri kwa kichwa na Bocco, lakini beki mmoja wa Rabat akaiwahi kwenye chaki na kuiondosha kwenye eneo la hatari.

Kocha Muingereza, Stewart Hall alilazimika kuwagawia majukumu, Msaidizi wake, Kali Ongala na Meneja Jemadari Saidi kuwafariji wachezaji hao, ingawa haikusaidia.

“Bocco na Mwantika wapo katika hali mbaya, tumejitahidi sana kuwafariji kwamba hii ni hali ya kawaida katika mchezo, lakini wanatulia, ila baada ya muda, wanarudia katika hali ile ile,”alisema Kali.

Wachezaji hao walisaidiwa kutoka kwenye vyumba vya kubadilishia nguo hadi kwenye basi kurejea hotelini na pia kushushwa kuingilia hotelini, Golden Tulip hadi vyumbani mwao- na tangu hapo hawakuweza kutoka nje. 

Azam FC inaondoka leo asubuhi mjini hapa saa 4:00 kwa treni kwa saa za huku na saa 6:00 kwa saa za Tanzania kwenda Casablanca kuunganisha ndege hadi Dubai, ambako italala na kuondoka na asubuhi ya kesho moja kwa moja kurejea Dar es Salaam.

Azam itasafiri kwa saa mbili hadi Cassablanca ambako itapanda ndege ya shirika la Emirates, wadhamini wa Arsenal ya England kwa saa tisa hadi Dubai.

Kesho, Azam itatumia saa sita kutoka Dubai hadi Dar es Salaam, ambako itafika jioni.