WALIMU wanaotarajia kuhitimu taaluma ya ualimu ngazi ya Stashahada katika chuo cha Ualimu St. Aggrey kilichopo Jijini Mbeya, wamepewa ajira kabla ya kufanya mitihani yao.
Ajira hizo zimeahidiwa katika viwanja vya chuo hicho na Mkurugenzi wa shule ya Sekondari ya Perfect Vission ya Jijini Dar es Salaam, ambaye pia ni mkuu wa wilaya ya Mbozi mkoani hapa Dr. Michael Kadeghe.
‘’Natoa ajira kwa wanafunzi watatu wa Diploma waje pale kwenye shule yangu Perfect Vission, mkifika mwambie mkuu wa shule anipigie simu’’ alisema Dr. Kadeghe ambaye alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya nne ya chuo hicho.
Mbali na ahadi hiyo ya ajira, pia aliahidi kuwa mwalimu yeyote anayehitimu mwaka huu katika chuo hicho cha St. Aggrey atakayepangiwa wilaya ya Mbozi na kukubali kufundisha shule za vijijini atamkopesha trekta.
Akizungumzia suala la wanafunzi kufeli, alisema kuwa wanafunzi wengi wanafundishwa kukariri jambo ambalo pia ni moja ya sababu ya kufeli.
‘’Kuanzia mwakani wanafunzi wa darasa la kwanza mpaka darasa la tatu watakuwa wanasoma masomo matatu yaani KKK ikiwa na maana ya kusoma, kuandika na kuhesabu’’ alisema Dr. Kadeghe ambaye kitaaluma ni Mwalimu na kwamba Lugha ya Kiingereza ni lazima iwekewe mkazo.
Aidha aliwaasa maafisa elimu wa wilaya kuwa na lugha za staha kwa walimu wanaporipoti katika wilaya zao tofauti na sasa ambapo kuna malalamiko mengi kutoka kwa walimu wanaoaza kazi kuwa kuwa wanatolewa lugha zisizo na staha maofisini kutoka kwa baadhi ya maofisa elimu wa wilaya zao.
Kwa upande wa walimu tarajali wa chuo hicho, walisema kuwa katika chuo hicho walipata usumbufu wa upatikanaji wa maji hasa yanapokuwa yamekatika, pia kuna changamoto ya baadhi ya wazazi/walezi kushindwa kulipa ada kwa muda muafaka na kusababisha usumbufu kwa wanachuo husika kurudishwa nyumbani mara kwa mara kwenda kufuata ada, hivyo kupoteza muda wa masomo.
Mkuu wa chuo hicho Stuart Danda, alisema kuwa kutokana na shule nyingi za michepuo ya kiingereza kuanzishwa nchini na kuajiri walimu kutoka nje ya nchi, chuo chake kimeanzisha masomo maalum kwa walimu ambao watamudu kufundisha shule hizo.
‘’Mbali na kuanzisha program hiyo hapa St. Aggrey, chuo tumefanikiwa kutoa ajira kwa wahitimu kila mwaka na mwaka huu tunatarajia kuwabakiza baadhi ya wahitimu wa Elimu Awali, Stashahada ya elimu Awali na walimu wa Stashahada ya Sekondari. Hapa tunaisaidia serikali katika kukabiliana na tatizo la ajira’’ alisema Mwalimu Danda.
Meneja wa taasisi ya St. Aggrey Jackson Kamugisha Kamugisha, alisema kuwa serikali inapaswa kuangalia mfumo wa baadhi ya vyuo vikuu ulioanzishwa wa kuwahadaa baadhi ya wazazi kuwa zinafundisha masomo ya elimu ya Sekondari wakati vyuo hivyo haviko katika mfumo wa Necta.
Akishukuru kwa niaba ya taasisi, Makamu Mkurugenzi wa taasisi hiyo Neema Mwambusi, alisema kuwa ahadi za ajira alizotoa Dr. Kadeghe ni chachu kubwa na kivutio cha wanataaluma hao huku akiwaasa wahitimu kuwa wakipangiwa vijijini wanapaswa kwenda kufundisha.