WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili kwa zaidi ya wiki nne umebaini kwamba kazi ya kubomoa nyumba hizo inaweza kuanza wakati wowote ingawa kuna changamoto kubwa kwani baadhi ya nyumba hizo ni za vigogo wenye madaraka makubwa serikalini au ndani ya vyama vya siasa. Habari zaidi zinadai kwamba baadhi ya vigogo hao wamekimbilia mahakamani kufungua kesi ya kupinga nyumba zao zisiguswe wakati wengine wamekua wakitoa vitisho kwa waliopewa mamlaka ya kuzibomoa
Wananchi hao wamemueleza waziri kwamba nyumba hizo zimeziba mkondo wa maji katika baadhi ya mito inayoingia baharini, hivyo kusababisha maji kuhama na kuelekea kwenye nyumba zao na daraja la eneo la Malecela kusombwa na maji hivyo kusababisha magari kutopita. Walidai kuwa nyumba nyingi zimejengwa katikati ya mto na wengine wamejaza vifusi kando ya mto unaopita karibu na nyumba zao, hivyo kusababisha mkondo wa maji kwenda kwa wananchi.
Vyanzo vyetu vya habari vinadai kwamba baadhi ya nyumba hizo zina hati zilizopatikana serikalini wakati zingine wamiliki wao walivamia maeneo hayo na kuporomosha maghorofa makubwa. Kutokana na ujenzi huo holela, wakazi wa Kawe kwa Malecela waliamua kumwandikia barua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakitoa malalamiko juu ya ujenzi huo.Barua hiyo ambayo gazeti hili lina nakala yake iliyoandikwa Februari 20, mwaka huu iliel eza kwamba ujenzi wa nyumba hizo umekuwa ni kero kubwa kwani zimejengwa katika mkondo wa maji hivyo mvua inaponyesha inasababisha mafuriko kwa wananchi wengine.
“Hivi sasa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam wanashindwa kutembelea ufukwe wa bahari kutokana na baadhi ya nyumba kuziba njia na mbaya zaidi waliojenga kando ya mkondo wameharibu mikoko,” imesema sehemu ya barua hiyo. Waliendelea kusema kwamba vigogo hao ambao ni wavamizi baadhi yao wamekuwa wakitembea na bastola hadharani na kuwatishia maisha wale wanaodiriki kuzungumzia ujenzi wanaoufanya katika maeneo hayo.
Wananchi hao wametishia kuwa endapo hawatasikilizwa wataenda Ikulu kumuona Rais Jakaya Kikwete. Kaimu Mkurugenzi wa Baraza la Hifadhi ya Mazingira nchini (NEMC), Ignas Mchallo alisema: “Wote waliojenga katika maeneo hayo watahamishwa kwa kufuata sheria kwani kuna wengine waliojenga kabla ya sheria ya mazingira ambayo inataka kuwepo kwa nafasi ya mita 60 toka mtoni au ufukweli,” alisema Mchallo.
Naye Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka alisema kwamba nyumba 73 zilizojengwa kwenye fukwe za Bahari ya Hindi, zitavunjwa na akazitaja kuwa ziko kwenye fukwe za Kawe, Mbezi na Msasani na kwamba ingawa zilijengwa kihalali baada ya kupewa hati, lakini sheria mpya hairuhusu nyumba hizo kuwepo.
(Picha na GPL)