Sunday, 28 April 2013

DIWANI WA CUF AJISALIMISHA MBELE YA WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI


diwani wa kata ya malunga john chagula akiwa kwenye moja ya mikutano yake.

Diwani wa Kata ya Malunga wilayani Kahama mkoani Shinyanga John Chagula, leo amelazimika kurudisha kiwanja alichomiliki katika eneo lenye mgogoro la Igomelo kufuatia malalamiko ya wananchi.

Hayo yametendeka leo kwenye ziara ya Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Goodluck Ole Medeye kutembelea maeneo yaliyoporwa kinyemela na kubadilishiwa matumizi mjini Kahama.

Dhoruba hiyo ilimkumba Chagula baada ya wananchi wa eneo hilo lililokuwa limepangwa kujengwa Soko, Kituo cha Polisi na makanisa kudai mbele ya Ole-medeye kwamba baadhi ya viongozi hasa madiwani wamejigawia eneo hilo huku wakijua ni la huduma za jamii.

Alipotakiwa kujieeleza, Chagula alitamka mbele ya hadhara kwamba anarudisha mara moja kiwanja hicho alichokijenga baada ya kuwa amepotoshwa na idara ya ardhi kwamba ni sehemu ya makazi.

Wengine walioagizwa kusalimisha viwanja hivyo ni pamoja na Diwani wa Kata ya Kahama mjini Abas Omari, Mkuu wa Wilaya ya Kahama Mstaafu Meja Matala na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Kata ya Malunga Donald Igulu.

Olemedeye amekuja Kahama kwa mwaliko wa Mbunge wa Jimbo la Kahama James Lembeli kwa ajili ya kujionea migogoro ya ardhi mjini kahamaambapo amefuta viwanja vyote vilivyotolewa kinyemela na watendaji wa idara ya ardhi wilayani humo.