Sunday, 28 April 2013

CCM WATOA TAMKO VURUGU ZA CHUO CHA UHASIBU ARUSHA


Chama Cha Mapinduzi(CCM) mkoani Arusha kimelitaka jeshi la polisi mkoani hapa sanjari na vyombo mbalimbali vya usalama kufanya uchunguzi wa kina na haraka ili kubaini chanzo cha kifo cha mwanafunzi wa chuo cha uhasibu Arusha (IAA),Henry Kago(22)  aliyefariki hivi karibuni baada ya  kuchomwa kisu na watu wasiojulikana.
Pia,chama hicho kimeitaka serikali kusimamia na kumaliza haraka uchunguzi ambao utawezesha shughuli za kimasomo kuendelea katika chuo hicho  na kutaka wale wote waliohusika na vurugu hizo wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari katibu mwenezi wa chama hicho mkoani Arusha,Isaack Joseph maarufu kama Kadogoo alisema kuwa chama chao  kinalaani vikali tukio la vurugu zilizojitokeza katika chuo hicho na kimepokea kwa masikitiko makubwa kifo cha mwanafunzi huyo.
Alisema kuwa tukio la kuuwawa kwa mwanafunzi huyo ni tukio la kinyama na waliotekeleza hawakujali uhai wa kijana huyo ambaye alikuwa ni nguvu kazi ya taifa  na kuitaka serikali kuwabaini waliohusika mara moja.
“Chama kimefikia hatua hiyo kutokana na tukio hilo la kinyama linalodaiwa kufanywa na watu wasiojali uhai wa watu wengine hususani kijana ambaye ni nguvu kazi ya taifa”alisema Joseph
Alisema kuwa wao kama chama wanaitaka serikali kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama kuchunguza kwa kina taarifa za tukio hilo ili kubaini ukweli na kuwachukulia hatua wahusika wote waliopanga mauaji ya mwanafunzi huyo.
Hatahivyo,alisisitiza kwa kuitaka serikali kusimamia na kumaliza haraka uchunguzi ambao utawezesha shughuli za kimasomo kuendelea chuoni hapo na kuwataka wanafunzi wa vyuo mbalimbali nchini kutambua kile kilichowapeleka chuoni hapo.
“Chama kinawaonya  wanafunzi wote katika vyuo mbalimbali nchini kutambua kilichowapeleka katika vyuo hivyo na kuachana na ushawishi wa wanasiasa wanaowaondoa katika malengo yao ya msingi ya kujipatia elimu”alisisitiza Joseph
Hatahivyo,alilipongeza jeshi la polisi mkoani Arusha kwa kazi nzuri ya kulinda raia na mali zake  hususani katika tukio la vurugu lililojitokeza chuoni hapo huku akidai wao watendelea kutoa ushirikiano kwa ufanisi na uweledi mkubwa.
JAMII BLOG