WATU 123 wamefikishwa mahakamani jijini Dar es Salaam katika kipindi cha miezi mitatu tangu Januari hadi mwezi uliopita wakishitakiwa kwa ukahaba.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angellah Kairuki alisema kesi 22 zikihusisha watu hao 123, zilifikishwa katika Mahakama ya Sokoine Drive maarufu kama Mahakama ya Jiji.
Alijibu kwa niaba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kairuki alikuwa akijibu maswali ya Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM) aliyetaka kufahamu serikali ina mpango gani wa kuleta muswada wa sheria ya kudhibiti ukahaba nchini kama ilivyofanyika katika nchi nyingine kama vile Afrika Kusini.
Mbunge huyo alisema kutokana na kutokuwepo sheria ya kudhibiti wanaofanya ukahaba, polisi inapowakamata huwaachia huru. Katika swali la msingi, mbunge aliendelea kuhoji, “Je, Serikali ina mpango gani wa kutoa elimu kwa makahaba ili waweze kutambua athari za tabia hiyo na wajue thamani waliyo nayo.”
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Kairuki alisema mpango wowote wa kutunga sheria kama ilivyofanyika katika nchi nyingine, utafanyika kama patatokea matokeo ya tathmini kuonesha upungufu wa mfumo wa sheria uliopo wa kushughulikia vitendo vya ukahaba.
Kwa mujibu wa Kairuki, kwa sasa vifungu vya 146, 148 na 149 vya Kanuni ya Adhabu vinaharamisha kitendo cha mwanamke kuishi kwa kutegemea mapato ya ukahaba na kusaidia kufanyika kwa vitendo hivyo kwa kutoa mahala pa kufanyia vitendo hivyo au kula njama ya kuwezesha kufanyika.
Adhabu ya mtu anayevunja sheria ni pamoja na kutumikia adhabu ya kifungo jela kisichozidi miaka miwili au kulipa faini na kifungo cha miaka mitatu jela.
Mbali ya hatua zinazochukuliwa na vyombo vya sheria, Kairuki alisema serikali inaendelea kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kuelimisha jamii, wakiwemo wanaume na makahaba watambue athari za tabia hiyo na wafahamu thamani waliyo nayo.
Miongoni mwa mashirika hayo ni Shirika la Kiota Women and Health Development (Kiwohede) ambalo limekuwa likiwaondoa wasichana makahaba kwenye maeneo wanayofanyia shughuli hizo haramu na kuwaelimisha madhara yake.
Shirika hilo limekuwa likiwapatia stadi mbalimbali zinazowawezesha kujitegemea na kuachana na vitendo hivyo. Stadi wanazopatiwa ni pamoja na ufumaji, utengenezaji wa batiki, usindikaji wa vyakula na ushonaji.
Vile vile shirika limekuwa likiwaendeleza kielimu na baadhi yao wanajiunga na Vyuo vya Ufundi (Veta). Hadi sasa zaidi ya vijana 40,000 wamefaidika na huduma za Kiwohede.
Mbunge Magige katika swali la nyongeza, pamoja na kutaka kufahamu idadi ya kesi zilizofikishwa mahakamani kuhusu makahaba, alishutumu kwamba adhabu zinazotolewa ni ndogo.
Akimjibu, Naibu Waziri alisema vitendo vya ukahaba vinakwenda mbali zaidi ya sheria kutokana na kuchochewa pia na sababu za kijamii. Aliwataka pia wanaume wanaowafuata kuacha kufanya hivyo.
Alisema adhabu wataiangalia kwa makini kwani washitakiwa wengi wanajirudia.
habari leo credited