Saturday, 11 May 2013

WANANCHI MAKETE MJINI WAOMBA VIFUSI KWENYE BARABARA ZA MITAA VISAMBAZWE

Moja ya barabara za mitaa kata ya Iwawa Makete mjini zikiwa zimelundikwa vifusi kwa zaidi ya miezi mitatu sasa huku kukiwa na kibao kikionesha barabara imefungwa ilihali magari yanapita hivyohivyo licha ya maelekezo ya kibao hicho
 
Vifusi vikiwa vimelundikwa barabara ya kuelekea hospitali ya wilaya ya Makete 
 
Hapa inalazimu magari kupita kwenye mifereji
 
 Vifusi vingine hadi vimeyeyuka kutokana na kukaa muda mrefu
 

Wananchi wa kata ya Iwawa wilayani Makete ambao ni watumiaji wakubwa wa barabara za mitaa katika kata hiyo, wameiomba halmashauri ya wilaya ya Makete kusambaza vifusi vilivyopo katika barabara hizo ambavyo vimewekwa zaidi ya miezi mitatu sasa

Wananchi hao wametoa ombi hilo kufuatia adha wanayoipata hasa wanapotumia magari kwa kuwa barabara hizo zimekuwa nyembamba hivyo kuleta usumbufu kwa watumiaji hasa wakati wa magari kupishana

Mmoja wa mwananchi aliyezungumza na ripota wetu Bw. Sipati Mbwilo amesema wanashangaa vifusi hivyo kukaa muda mrefu barabarani bila kusambazwa, jambo linalosababisha usumbufu kwa watumiaji na wakati mwingine kulazimika kuzunguka kupita kwenye barabara nyingine ili kufuata huduma hata kama huduma hiyo ipo jirani

“Unajua braza unaweza kukuta umepata kazi ya kupeleka kuni ama kwenda kuchukua kuni kwa gari, lakini inakulazimu uzunguke umbali mrefu ili kukwepa hivi vifusi ambavyo hatujui vitasambazwa lini, ni bora wangeviweka pindi watakapokuwa tayari kuvisambaza leo mwezi wa tatu vifusi vipo barabarani mambo gani haya” alisema Mbwilo

Naye dereva wa lori aliyejitaja kwa jina la Kisauti amesema vifusi hivyo vinawapa tabu wanaoendesha magari makubwa kutokana na wembamba wa barabara na wakati mwingine kulazimika kukataa baadhi ya kazi wanazozipata kutokana na magari yao kushindwa kupita kwenye barabara hizo

Ripota wetu amezungumza na mhandisi wa ujenzi wilaya ya Makete Mhandisi Samwel Ndoveni ambaye amekiri kuwepo hali hiyo lakini amesema kero hiyo itaondolewa hivi karibuni kwa kuwa msimu wa mvua uliokuwa ukikwamisha utekelezaji wa zoezi hilo unamalizika na mkandarasi ataanza kazi mara moja

Amesema kwa mwaka huu mvua zilinyesha kwa wingi na ndiyo maana zoezi hilo lilishindwa kutekelezeka kwa wakati kama ofisi yake ilivyokuwa imepanga

“Ni heri lawama za kutokusambaza vifusi zitupate kuliko tungesambaza vifusi wakati mvua inanyesha, matokeo yake tungetengeneza tope jingi na barabara zisingepitika huo ungekuwa ni uharibifu wa fedha za serikali” alisema Mhandisi Ndoveni