Saturday, 4 May 2013

TUNDU LISSU AMLIPUA DK MIGILO, AFUNGUKA MAZITO. SOMA ALICHOKISEMA HAPA

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imesema ina ushahidi unaoonyesha njama za kuhakikisha kuwa ni wana CCM pekee, ndiyo watakaochaguliwa kuwa wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya kwa upande wa Tanzania Bara.
Imedai kuwa njama hizo zimepangwa na ngazi za juu za chama hicho.
 
Akitoa maoni upinzani, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kuhusu Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, alisema Machi 3, mwaka huu siku mbili baada ya Mwongozo wa Tume kuanza kutumika, Katibu wa NEC ya CCM (Uhusiano wa Kimataifa), Dk Asha-Rose Migiro alituma barua pepe kwa wajumbe na watendaji wa Sekretarieti ya NEC-CCM inayoonyesha kujipanga kuingia kwenye mabaraza peke yao.
 
“Barua pepe ya Dk Asha-Rose Migiro inasema “Sambamba na hatua za awali tulizochukua baada ya kupata rasimu ya mwanzo ya Mwongozo wa Tume, sasa tunatakiwa tuongeze juhudi za ushiriki wetu na kutayarisha makundi husika kama tulivyokwishaongea,” Lissu alinukuu barua pepe hiyo.
 
Lissu alisema baada ya Dk Migiro kuagiza alimalizia kwa maneno yafuatayo: “Tafadhali wanakiliwa msisite kutoa maoni, ushauri na mbinu bora zaidi za kutimiza azma yetu katika suala hili muhimu.”
 
Aliwataja waliopelekewa nakala ya barua pepe ya Dk Asha-Rose Migiro, kuwa ni Mwigulu Nchemba, Zakhia Meghji, Muhammed Seif Khatib na Nape Nnauye.
 
Lissu alisema siku moja baadaye, Nape aliwaandikia ‘wanakiliwa’ wenzake akiwashauri ikiwezekana kwa sababu ya unyeti wa suala hilo, wapate taarifa kila siku kuhusu hali halisi inavyoendelea katika kila mkoa na kwamba ni vizuri idara ikaandaa orodha ya mambo muhimu ya kupima kama mchakato unakwenda vizuri au la!
 
Alisema njama za CCM kuteka nyara mchakato pia zinahusu uhalalishaji wa Katiba Mpya kwenye kura ya maoni na kwamba, Desemba 18, mwaka jana, Katibu wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Francis Mwonga, aliwaandikia barua makatibu wote wa CCM wa mikoa na kuwapa maelekezo ya kikao cha Sekretarieti.
 
“Wakati wa kupiga kura ya maoni kuhusu Katiba Mpya mawasiliano yafanywe na wahusika ili vituo vya kupigia kura visiwe mbali sana na wananchi,” alisema Lissu akimkariri Mwonga.
 
Lissu alisema maneno hayo yaliandikwa hata kabla Tume haijamaliza zoezi la kukusanya maoni ya wananchi, tayari Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM inawaelekeza makada wake mikoani, kufanya mawasiliano na ‘wahusika’ kuhusu jinsi ya kupanga vituo vya kupigia kura.
 
Alisema mawasiliano hayo ya viongozi wa ngazi za juu za CCM, yanathibitisha kuwa mchakato wa Katiba Mpya umeingiliwa na kuhujumiwa kwa kiwango kikubwa na CCM.
 
Pia, alisema mawasiliano hayo yanathibitisha kauli iliyotolewa bungeni na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, wakati wa mjadala wa hoja ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwamba viongozi wa Serikali walihamasisha wenyeviti wa vijiji, mitaa na madiwani kuhakikisha kuwa wagombea wote wasiokuwa wa CCM, hasa wa Chadema wanaenguliwa chaguzi za vijiji, mitaa au kata.
Washtukia bajeti Tume ya Katiba Mpya
Tume hiyo iliombewa kuidhinishiwa Sh33.944 bilioni sawa na kiwango kilichoidhinishwa mwaka jana, kwa ajili ya matumizi mwaka 2013/14, Sh2.193 bilioni kwa ajili ya kulipia posho za vikao kwa wajumbe 34 na 160 wa sekretarieti.
 
Lissu alisema Sh1.728 bilioni zitalipia posho ya kujikimu kwa ajili ya wajumbe na sekretarieti wanaposafiri ndani ya nchi na Sh1.650 bilioni kwa ajili ya kulipa gharama za nyumba kwa wale wanaotoka nje ya Dar es Salaam.
 
Mbunge huyo alisema kuna Sh18 milioni zinazoombwa kugharamia chakula kwa wajumbe wa tume na sekretarieti watakaokuwa wamepata maambukizi ya Ukimwi.
 
Pia Sh60 milioni kwa ajili ya usafiri wa ndani, Sh50 milioni gharama za malazi kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wanaposafiri kikazi.
 
“Sh423 milioni za chai na vitafunwa na Sh50 milioni za wahudumu wanaosaidia kazi za tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye Mabaraza ya Katiba na zoezi la upigaji kura ya maoni,” alisema.
 
Alisema Sh60 milioni zinatakiwa kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za tume, Sh30 milioni za kulipia gharama za usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe na sekretarieti watakaposafiri ndani ya nchi kikazi na Sh103 milioni za kulipia gharama za simu za mikononi.
 
“Ulaji huu mwingine unajumuisha Sh604 milioni za posho kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa Bunge Maalumu la Katiba. Maelezo ya tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘hardship allowances’, yaani posho ya mazingira magumu, wakati vikao vya Bunge Maalum la Katiba vitafanyika Dar es Salaam au hapa Dodoma!” alisema.
 
Pia, alisema kwenye ulaji huo mpya kuna Sh266 milioni za chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalum la Katiba na Sh12 milioni kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa shughuli zinazohusiana na Tume.
 
Hali kadhalika Sh185 milioni za usafiri wa basi na teksi na Sh30 milioni za kutengeneza fulana na kofia kwa wajumbe wa tume na sekretarieti.
 
“Sh19.039 bilioni zinaombwa kwa ajili ya posho za aina mbalimbali na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na sekretarieti ya tume kwa mwaka wa fedha 2013/14. Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya bajeti yote inayoombwa kwa ajili ya tume.
 
Kwa ulinganisho, posho na malipo mengine yanayowahusu wajumbe na sekretarieti ya tume yalikuwa Sh14.633 bilioni au asilimia 43 ya bajeti yote ya mwaka wa fedha uliopita,” alisema Lissu na kuongeza:

“Hii ina maana kwamba gharama za moja kwa moja za wajumbe na sekretarieti ya tume zitaongezeka kwa zaidi ya Sh4.406 bilioni au zaidi ya asilimia 30 ya gharama za mwaka jana kama Bunge litaidhinisha maombi haya,” alisema Lissu.