Hali ya taharuki ililikumba Jiji la Dar es Salaam jana baada ya  kuwapo kwa taarifa za kulipuliwa kwa bomu katika Kanisa la Kiinjili la  Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kunduchi Mtongani, Manispaa ya  Kinondoni.
Taarifa hizo zilisambaa katika mitandao ya kijamii  na baadhi ya vyombo vya habari na kuwafanya wananchi kujiuliza nini  kinalikumba taifa katika kipindi hiki.
Hali hiyo ya taharuki na mshtuko kwa wananchi  inatokana na shambulio la bomu katika Kanisa Katoliki la Mtakatifu  Joseph Mfanyakazi la Parokia ya Olasit jijini Arusha, lililotokea  Jumapili iliyopita na kusababisha vifo vya watu watatu na majeruhi 67.
Hata hivyo, taharuki ya jana ilisababishwa na  Jeshi la Polisi Mkoa wa Kinondoni kufyatua mabomu ya machozi walipokuwa  wakitekeleza operesheni ya kukamata wahalifu waliokuwa katika majengo  mawili mali ya Kanisa la KKKT, Kunduchi Mtongani.
Katika kutekeleza operesheni hiyo polisi hao  walifunga njia zote tatu za kutoka na kuingia eneo hilo ili kuhakikisha  vibaka hao hawakimbii.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Samweli Nzuna alisema kuwa baada ya kuona wanakaribia eneo hilo, polisi walifyatua juu mabomu ya machozi yaliyotoa mlio mkubwa ili kuwachanganya wahalifu waliokuwa katika majengo hayo ya kanisa wakicheza kamari na kuvuta bangi.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Samweli Nzuna alisema kuwa baada ya kuona wanakaribia eneo hilo, polisi walifyatua juu mabomu ya machozi yaliyotoa mlio mkubwa ili kuwachanganya wahalifu waliokuwa katika majengo hayo ya kanisa wakicheza kamari na kuvuta bangi.
Alisema mara baada ya polisi hao kufyatua mabomu  hayo wananchi waliokuwa karibu na eneo walianza kukimbia ovyo wakidhani  jengo la kanisa limelipuliwa na vibaka hao walikimbia kuelekea katika  mikoko iliyo mkabala na kanisa kabla ya polisi kufyatua tena bomu la  machozi ili kuwazuia vibaka hao kukimbia zaidi.
“Wakati wa utekelezaji wa operesheni hiyo hakuna  mwananchi yeyote aliyeumia ila walishtuka na wengine kudhani kuwa kanisa  lilikuwa limelipuliwa kwa bomu na wahalifu, kwani awali hawakujua kama  waliofanya hivyo ni polisi,”alisema Nzuna.
Naye Aloys Mwamanga, mkazi wa eneo hilo ambaye pia  ni Rais wa Shirikisho la Wenye Viwanda na Kilimo nchini (TCCIA),  alisifu operesheni hiyo akisema:
“Vibaka hawa wamekuwa wakisumbua kwa kipindi  kirefu eneo hili, wameniibia hata runinga yangu hivyo naona hivi sasa  amani itarejea eneo hili.”
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni,  Charles Kenyela alikiri tukio hilo akisema kuwa kwa sasa jeshi lake  linaendesha operesheni kali ya kuwasaka wahalifu wote.
“Hivi sasa tupo katika kipindi kigumu ukilinganisha na tukio lililotokea Arusha.
Tutahakikisha mkoa wa Kinondoni unakuwa katika hali ya usalama na wananchi watupe ushirikiano,”alisema Kamanda Kenyela.
                               Alisema kuwa taarifa za kulipuliwa kwa bomu kwa  kanisa hilo la KKKT hazina ukweli wowote bali kilichotokea ni kuwakamata  wahalifu waliokuwa wakiendesha vitendo vya kuhatarisha amani katika  majengo pacha yanayomilikiwa na kanisa hilo, yakiwa kama mapango  yasiyokaliwa na watu kwa kipindi kurefu.
                               Alisema katika operesheni hiyo polisi walitumia mabomu ya machozi baada ya vibaka hao kukimbilia eneo la kanisa na baharini.
                               “Baada ya kupiga mabomu ya machozi, waumini  waliokuwa kanisani walitaharuki na kufikiri linalipuliwa, hiyo inatokana  na kilichotokea Arusha. Lakini baada ya kuona polisi wakiwakimbiza  vibaka hao, waumini nao waliwasaidia kuwatia nguvuni,”alisemaKamanda  Kenyela na kuongeza:
                               “Vibaka hao walikuwa wakihatarisha usalama wa eneo  hilo kwani walikuwa wakicheza kamari, kuvuta bangi na kupanga vitendo  vya kihalifu walivyokuwa wakivitekeleza nyakati za usiku.”
                               Alisema kuwa operesheni hiyo imewatia mbaroni watu  sita, kati yao akiwamo mtoto wa miaka 13, mwanafunzi wa kidato cha nne  wa Shule ya Sekondari Boko, Mwanafunzi wa Chuo cha Komputa wa Chuo Kikuu  cha Dar es Salaam tawi la Mbezi na kondakta wa daladala.
                               “Hivi sasa tuna msako mkali sana na wananchi walio  wema wasiogope kwani tumewakamata wahalifu wengi na siku yoyote Kamanda  wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam Suleiman Kova atatoa orodha yake na  matukio waliyoyafanya,” alisema Kamanda Kenyela.
                               Maeneo mengi ya jiji la Dar es Salaam hususan ya  Manzese, Vingunguti, Buguruni, Mbagala, Kariakoo na maeneo mengine yana  vibaka wengi aambao wamekuwa wakishiriki katika vitendo vya uhalifu  mchana na usiku bila ya kuchukuliwa hatua.
mwananchi
mwananchi