Monday, 20 May 2013

MWANDAMIZI WA POLISI ARUSHA AKAMATWA NA MAGUNIA 18 YA BANGI.....

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Said Mwema 


Gari aina ya Toyota Landcruiser linalotumiwa na Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Arusha, lilikamatwa juzi mjini Moshi likiwa limesheheni magunia 18 ya bangi.
 
Habari za awali zilieleza kuwa gari hilo lilikamatwa juzi saa 4:00 usiku katika Mji mdogo wa Himo, Moshi Vijijini likisafirisha bangi hiyo kwenda Tarakea, Rombo.
 
Polisi wawili akiwamo dereva wa gari hilo wanashikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Himo na gari lipo Makao Makuu ya FFU, Moshi.
 
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kukamatwa kwa askari hao: “Mchakato wa kuwafikisha mahakama ya kijeshi unaandaliwa. Bangi hiyo ilikuwa inapelekwa kwa mfanyabiashara mmoja huko Rombo na ndiye aliyewakodi.”
 
Hata hivyo, Kamanda Boaz alisema atatoa taarifa zaidi leo kwani uchunguzi bado unaendelea.
 
Bangi ilivyonaswa
Habari zimeeleza kuwa polisi waliokuwa doria waliliona gari hilo likitengenezwa na waliamua kuwauliza wenzao kulikoni? Wakajibiwa kuwa kuna kitu walikuwa wakirekebisha na lilikuwa ni tatizo dogo tu.
 
“Walipoulizwa kwani mnaelekea wapi wakasema wanapeleka mzigo wa bosi huko Tarakea mpakani na kwa taratibu zetu za kijeshi huwezi kuuliza ni bosi gani,” kilidokeza chanzo kimoja ndani ya polisi.
 
Hata hivyo, polisi hao wa doria walirudi katika gari yao ili waendelee na doria lakini baadhi ya polisi wakamweleza ofisa aliyekuwapo katika gari hilo kwamba wanashuku gari lile limebeba bangi.
 
“Lilikuwa na harufu kali ya bangi na hilo ndilo lililowafanya wale polisi kurudi tena kwa wenzao na kuwaambia wanataka waone wamebeba nini ndipo wakakutana na magunia 18 ya bangi,” kilieleza chanzo chetu.
 
Inadaiwa kuwa baada ya kukuta bangi hiyo, polisi hao waliwasiliana na Mkuu wa Upelelezi (RCO), Mkoa wa Kilimanjaro, Ramadhan Ng’anzi ambaye naye alimjulisha Kamanda Boaz.
 
Ilielezwa kuwa Kamanda Boaz aliagiza kuwekwa mahabusu kwa polisi hao katika Kituo cha Himo na gari hilo lipelekwe FFU, Moshi.
 
Ofisa mmoja wa Polisi alidokeza kuwa baada ya kukamatwa, polisi hao waliwasiliana na kigogo mmoja wa polisi Arusha ambaye inadaiwa aliwafokea kwa kukamatwa kizembe.
 
“Inaonekana wanafanya sana biashara hiyo kwa sababu karibu kila siku hili gari limekuwa likipita hapa. Hao jamaa walitaka kuwahonga wale polisi Sh500,000 lakini walikataa,” alisema ofisa huyo.
 
Arusha
Watanzania watatu wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro, Arusha waliuawa kwa tuhuma za ujambazi huko Narok, Kenya Mei 2, mwaka huu na kukutwa na bunduki aina ya ‘Sub Mashine Gun’ (SMG) ambayo inasadikiwa kuwa ni mali ya Jeshi la Polisi Tanzania.
 
Silaha hiyo ilitakiwa kuwa imehifadhiwa kwenye ghala la silaha katika Kituo cha Polisi Loliondo.
 
Kutokana na tukio hilo la aina yake, askari wawili wa Kituo cha Loliondo, ambao majina yanahifadhiwa wanashikiliwa na polisi wilayani Ngorongoro kwa uchunguzi kutokana na kupotea kwa silaha hiyo hadi kukutwa mikononi mwa majambazi.
 
“Ni kweli tukio hili limetokea na kuna polisi wanahojiwa kutokana na upotevu wa bunduki hiyo,” Mkuu wa Wilaya hiyo, Elias Wawa Lali alisema.
 
Imeelezwa kuwa Watanzania hao waliuawa katika tukio la kuwateka wafanyabiashara wa Kenya waliokuwa wanatoka mnadani na kuwapora.
 
Lali alisema katika tukio hilo, majambazi hao waliwaua wafanyabiashara wawili, lakini baadaye walizingirwa na wananchi na wakauawa na kukutwa na bunduki hiyo.
 
Majambazi hao, waliouawa wametajwa kuwa ni Tigiki Pasto, Steven Webo na mwingine aliyejulikana kwa jina moja la Kadogoo, wote wakazi wa Wilaya ya Ngorongoro.
 
Hata hivyo, alieleza kushangazwa na hatua ya ndugu wa marehemu majambazi hao kushindwa kwenda Kenya kuchukua miili ya ndugu zao kwa ajili ya mazishi hadi jana.
 
“Sisi kama Serikali tulijitahidi kuhakikisha miili ya hawa waliouawa inaletwa nchini kuzikwa lakini hawa ndugu cha ajabu wanataka polisi ndiyo wakawaletee miili,” alisema.
 
Mmoja wa ndugu wa marehemu hao, ambaye aliomba kutokutajwa jina alisema wameshindwa kwenda kuchukua miili hiyo kwa sababu za kiusalama.
 
Alisema katika mazingira ya sasa ya Wilaya ya Narok kama wangekwenda huenda wangeuawa.
 
Hata hivyo, Mkuu wa Ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi la Polisi, Isaya Mngulu na Kamanda wa Polisi wa Arusha, Liberatus Sabas walidai kuwa hawana taarifa ya tukio hilo.
 
Kuuawa kwa majambazi hao, pia kumekuja wakati kukiwa na taarifa za muda mrefu za Polisi Wilaya ya Ngorongoro kuwasaka majambazi hao kutokana na kuhusika katika matukio kadhaa ya ujambazi katika maeneo ya Mji wa Wasson na Vijiji vya Soitsambu.
 
Imeandikwa na Daniel Mjema, Mussa Juma na Boniface Meena.   
 
MWANANCHI