Saturday, 11 May 2013

MKUU WA MKOA WA NJOMBE ATEMBELEA WACHIMBAJI WADOGO WILAYANI LUDEWA

Mkuu wa mkoa wa Njombe kapteni mstaafu Assery Msangi jana aliwatembelea wachimbaji wadogo wa madini wilayani Ludewa ikiwa ni moja ya ziara yake ya kutambua aina ya madini yanayopatikana wilayani humo.
 
Katika ziara hiyo Kepteni Msangi aliweza kutembelea machimbo ya dhahabu na shaba katika kata ya Nkomang’ombe eneo la Muhumbi ambako aliweza kuongea na wananchi pamoja na wachimbaji wadogo ambao waliweza kutoa kero mbalimbali zinazowakabili na baadae kwenda machimbo ya dhahabu yaliyoko kijiji cha amani kata ya Mundindi.
 
Akiongea na wananchi pamoja na wachimbaji wadogo Kamteni Msangi aliwasisitiza wananchi hao umuhimu wa kuwapeleka watoto wao shule ili waje kuwa warithi wazuri wa machimbo hayo.
 
“ni vema watoto wenu wakapata elimu ili waje kunufaika na migodi hii kuliko kuishi nao polini bila ya kuwapeleka shule lakini katika migodi ndiko maambukizi ya ukimwi yanakoshamili hivyo mnatakiwa kuwa waangalifu katika kazi zenu”,alisema Kapteni Msangi.
 
Kapten Msangi alisema mkoa wa Njombe unaongoza katika maambukizi ya virusi vya Ukimwi nchini hivyo kila mchimbaji anatakiwa kuwa mwangalifu kwani sio sifa nzuri kuongoza kwa jambo hilo bali kushirikiana kujitoa katika sifa hiyo mbaya.
 
Wilaya ya Ludewa inazaidi ya aina saba za madini ambapo kuna maeneo wamepewa wawekezaji wan je na maeneo mengine yamekaliwa na wawekezaji wa ndani ambao bado hawajaanza uchimbaji na kuyaacha maeneo hayo yakiwa misitu mikubwa.
 
Akitoa kero zinazowakabili wachimbaji wadogo John Hiluka alisema kumekuwa na mkanganyiko wa mipaka katika kata Nkomang’ombe kati ya wachimbaji wakubwa na wadogo hali ambayo inawanyima uhuru wachimbaji wadogo.
 
Bw.Hiluka alisema awali wanchi wa kitongoji cha Muhumbi walikubaliana na shirika la Maendeleo la Taifa(NDC)mwisho wa maeneo ya wawekezaji lakini cha kushangaza wawekezaji hao wamevuka mipaka na kuingia katika eneo wanaloishi wananchi.
 
Alisema eneo ambalo walipewa wawekezaji wa kampuni ya M.M.I lilikuwa ni lile lenye makaa yam awe lakini baada ya kuona eneo wanaloishi wananchi lina madini aina nyingine yakiwemo ya shaba na dhahabu ndiko waliko wachimbaji wadogo kampuni hiyo imevuka na kufika huko.
 
Bw.Hiluka alisema ni vema Serikali kupitia shirika la maendeleo la taifa(NDC) wakatenga mapema eneo la wachimbaji wadogo ili waweze kujipatia rizki kwani bila ya kufanya hivyo wachimbaji hao na wawekezaji wanaweza kusababisha madhara makubwa.
 
Nae msimamizi wa wacimbaji wadogo katika machimbo ya dhahabu Amani Bw.Samwel Kabelege alimwomba mkuu wa mkoa kuangalia upya mipaka ya eneo la wachimbaji wadogo katika eneo lao kutokana na eneo hilo kuwa finyu.
 
Bw.Kabelege alisema inasikitisha kila wanapotaka kupanua eneo la uchimbaji wanaambiwa na mamlaka kuwa maeneo yote yanawatu hali ambayo inayowafanya wachimbaji wadogo kurudia maeneo hay ohayo katika uchimbaji.
 
“inasikitisha kuona kila tukienda ofisi ya madini ya kanda mkoani Mbeya majibu tunayopata ni kwamba maeneo yote ya wilaya ya Ludewa yanawatu tayari wakati hayafanyiwi kazi,tunachokiomba kwa Serikali itutengee maeneo sisi wazawa wachimbaji wadogo badala ya kuyauza maeneo yote katika nchi yetu”,alisema Bw.Kabelege.
 
Aidha Mkuu wa wilaya ya Ludewa Bw.Juma Solomon Madaha aliwataka wachimbaji hao kuwa watulizu na kuyatoa malalamiko yao kwa maandishi ili yaweze kufanyiwa kazi kwani hakuna jambo lisiloweza kutatulika.
 
Bw.Madaha aliwahimiza wachimbaji hao kulipa kodi ili halmashauri iweze kupata mapato kwani kunawachimbaji wadogo wengi ambao wamejiunga katika vikundi mbalimbali lakini hawataki kulipa kodi licha ya kuwa wanazitumia barabra za halmashauri hiyo kusafirisha shaba.
 
Alisema wachimbaji wamekuwa wakikwepa kodi kwa kusingizia wanailipa wizara hali ambayo inainyima mapato Halmashauri,kwa kuangalia hilo hata ruhusiwa mchimbaji yeyote kupitisha madini yake bila kulipia ushuru