Thursday, 2 May 2013

MGOGORO WA SOKO LA MASHINE TATU MKOANI IRINGA WAENDELEA KUUNGURUMA

Wafanyabiashara wakiendelea na biashara katika soko la Mashine tatu Manispaa ya Iringa.

 Shaban Waziri- Katibu msaidizi wa Soko la Mashine tatu akizungumzia kero hiyo.
 
 Jafari Sewando- Mwenyekiti wa Soko la Mashine tatu akizungumzia hatua ya wafanyabiashara kugomea kulipa ushuru.

  Mfanyabiashara (mama Elia) akiwa anasubiri wateja katika eneo lake la biashara.
 
Ramadhan Waziri akitoa kero dhidi ya wenzao kuuza bidhaa nje ya Soko hilo na wao kukosa wateja.

LILE sokomoko la wafanyabiashara wa soko la Mashinetatu Mkoani Iringa limechukua sura mpya baada ya wajasiriamali wanaoendesha biashara zao ndani ya soiko hilo kugomea kulipa ushuru mkoani Iringa wamegoma kulipa -kwa madai ya kuwa wanapata hasara kwa kuwakosa wateja baada ya manispaa kushindwa kuwabana wafanyabiashara wanaouza nje ya masoko rasmi yaliyotengwa, na hivyo Manispaa kupoteza zaidi ya sh. 2.5 zinazokusanywa kwa mwezi sokoni hapo.

Wakizungumzia hatua ya wao kufanya hivyo, wafanyabiashara hao wamesema hawaoni sababu ya kulipa ushuru wa soko hilo wakati mali zao zinaoza  kila siku kwa kukosa wateja, baada ya wafanyabiashara wenzao kupanga bidhaa nje ya soko hilo na hivyo wateja kushindwa kuingia ndani ya soko.

"Sisi hatulipi ushuru, kwa sababu wenzetu wanaowadaka wateja huko nje barabara hawalipi ushuru, sie ambao tunaozesha tu mali zetu kwa kukosa wateja ndiyo tunalipa huo ushuru, sasa kuanzia leo hatutoi ushuru," Alisema Ramadhan Waziri.

Lucy Kifalu na Sofia Hello wamesema bidhaa zao kama Nyanya, Vitunguu na mbogamboga zimekuwa zikioza, na hivyo mitaji yao kukatika kila siku baada ya wenzao kufanya biashara katika eneo la barabara na hivyo wateja kushindwa kutoingia katika soko hilo.

Juliana Sanga amesema hata mikopo ya fedha waliyochukua katika benki ili kuendeshea biashara zao wanashindwa kurejesha, na hivyo kuwa katika hatari ya kunyang'anywa mali zao.

"Hapa tulipo tunamikopo, tulikopa kwa ajili ya kuzungusha mtaji wa biashara, lakini kutokana na hali hii ya wengine kufanya biashara nje ya soko hili, tena barabarani, kwa hiyo wateja hawaji humu sokoni, wanaishi huko nje, kwa hiyo sisi hatulipi ushuru mpaka wawaondoe wale wanaowadaka wateja pale nje," Alisema Juliana.

Ramadhan Nasoro na Maulisia Mbilinyi  nao wakasema kutokana na kudolora kwa biashara sokoni hapo, wanashindwa hata kurejesha  madeni ya mikopo ya fedha waliyokopa katika taasisi za kibenki, kutokana na biashara zao kukosa soko.

Aidha ofisi ya mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa kupitia mwanasheria wake, Innocent Kihaga amesema wataendesha zoezi la kuwakamata wale wote wanaokiuka sheria za masoko ya manispaa hiyo.