ALIYEKUWA kiungo wa kimataifa wa Rwanda, Patrick Muteesa Mafisango aliyechezea klabu mbili kubwa nchini, Azam na Simba SC zote za Dar es Salaam leo ametimiza mwaka mmoja tangu kifo chake kilichotokana na ajali ya gari maeneo ya Chuo cha Ufundi (VETA), Chang’ombe, Dar es Salaam (Jumatano Mei 16, 2012).
Mafisango alifariki kwa ajali ya gari akiwa anarejea nyumbani kwake, kutoka disko na baada ya ajali mwili wake ukahifadhiwa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Dar es Salaam.
Mafisango |
Meneja wa Simba SC, Nicodemus Menard Nyagawa ndiye aliyekuwa mtu wa kwanza kuipa habari za msiba huo BIN ZUBEIRY akisema hilo ni pigo kubwa kwa klabu hiyo.
Nyagawa alisema Mafisango aliyekuwa anaendesha mwenyewe gari lake, alikuwa anajaribu kumkwepa dereva wa pikipiki na kwa bahati mbaya akaingia mtaroni na kuumia kabla ya kufariki dunia.
Mafisango aliyekuja nchini mwaka 2010 na kujiunga na Azam kabla ya kuhamia Simba mwaka juzi, alizaliwa Machi 7, mwaka 1987 mjini Kinshasa, DRC alikoanzia soka kabla ya kuhamia Rwanda, ambako baadaye alichukua uraia wa nchi hiyo.
Kabla ya kuja Tanzania alichezea APR ya Rwanda.
Mechi ya mwisho Mafisango kuichezea Simba ilikuwa dhidi ya Al Ahly Shandy nchini Sudan katika hatua ya 16 Bora ya Kombe la Shirikisho, ambayo Simba ilitolewa kwa penalti 9-8, kufuatia sare ya jumla ya 3-3.
Wachezaji wa Taifa Stars, John Bocco kulia na Juma Nyosso wakiwa wamebeba jeneza la Mafisango kuliwasilisha TCC Chang'ombe |
Hadi anafariki dunia, Mafisango alikuwa ni tegemeo na siku moja kabla ya kifo chake, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geoffrey Nange Kaburu alisema kiungo huyo yupo kwenye mpango wa kocha wa kikosi cha msimu huu.
Mwili wa Mafisango uliagwa katika viwanja vya TCC Club, Chang’ombe, Dar es Salaam na kwenda kuzikwa kwao Lemba, nje kidogo ya jiji la Kinshasa, DRC.