Friday, 3 May 2013

KOCHA WA AZAM FC AMETAMBA YA KWAMBA LAZIMA WAWANG'OE WAARABU KATIKA MCHEZO WAO LEO KWANI AMEJIANDAA KWA KILA KITU

Kocha Stewart Hall akiwaongoza bijana wake mazoezini mjini hapa. Kila la heri Azam FC leo.

KOCHA wa Azam FC, Stewart Hall amesema kwamba amejiandaa kwa kila kitu kwa ajili ya mchezo wa leo wa marudiano Raundi ya Tatu Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji AS FAR Rabat, kwenye Uwanja wa Prince Moulay Abdellah.

Mchezo wa leo unaweza pia kuamuliwa kwa mikwaju ya penalti, iwapo timu hizo zitatoka sare nyingine ya bila kufungana kama Dar es Salaam wiki mbili zilizopita.

Akizungumza na mwandishi jana kwenye Uwanja wa Moulay Abdellah, Kocha huyo Muingereza alisema kwamba amejiandaa hadi kwa mikwaju ya penalti iwapo itatakiwa kuamua mshindi.

“Nimeandaa wapigaji tisa wa penalti, nimemuandaa kipa wa kudaka penalti. Nimejiandaa kwa ajili ya mchezo mzima na niko tayari kabisa,:”alisema.  

Akiizungumzia timu yake kwa ujumla, Stewart alisema morali ya wachezaji iko juu sana kuelekea mchezo huo na ana matumaini makubwa ya kufanya vizuri.

Alisema hakuna majeruhi hata mmoja kwenye timu na beki aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya bega, Joackins Atudo kwa sasa yuko fiti kabisa.

Kuhusu wapinzani wake, Stewart ameendelea kusistiza si timu ya kutisha baada ya kuiona tena ikicheza Alhamisi wiki hii katika ligi ya kwao mjini hapa na kushinda 1-0 kwa taabu dhidi ya Widad Fez.

Hata hivyo, Stewaert amesema FAR Rabat ambayo ni yimu ya jeshi nchini hapa, ina wachezaji watatu wazuri na hatari kwa timu yake, ambao ameahidi kuwawekea ulinzi wa uhakika wasilete madhara.

Kutakuwa na mechi nyingine ya Kombe la Shirikisho mjini Casablanca leo kati ya Wydad Casablanca na Liga Muculmana ya Angola. Mechi nyingine za mashindano hayo leo ni kati ya Ismailia na Al Ahli Shendi, Etoile Sahel na Recreativo da Caala, Diables Noirs na CS Sfaxien, LLB Academic na ASEC Mimosas, US Bitam na USM Alger na SuperSport United dhidi ya ENPPI.

Timu zitakazofuzu katika hatua hii, zitaungana na timu zitakazotolewa katika Ligi ya Mabingwa kucheza mechi maalum za mchujo kuwania nafasi ya kucheza hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho.

Ingawa Stewart hakuwa tayari jana kutaja kikosi chaje cha kwanza, lakini bila shaka kitakuwa hivi; Mwadini Ally, Himid Mao, Waziri Salum, David Mwantika, Joackins Atudo, Kipre Balou, Kipre Tchetche, Salum Abubakar, John Bocco, Humprey Mieno na Khamis Mcha ‘Vialli’. 

AS FAR Rabat; Ali Grouni, Mustafa Mrani, Younes Hammal, Younes Belakhdar, Yassine El Kordy, Abdelrahim Achchakir, Salaheddine Said, Mohamed El Bakkali, Salaheddine Aqqal, Mustafa Allaoui na Hicham El Fathi. Kila la heri wawakilishi wa Tanzania. Mungu ibariki Azam, ibariki Tanzania. Amin.