RASIMU ya Sera ya Elimu na Mafunzo nchini inapendekeza kuunganisha elimu ya msingi na sekondari ya kawaida ya sasa ili kuunda elimu-msingi itakayotolewa kwa kipindi cha miaka 10 kuanzia mwaka 2018, imefahamika.
Rasimu ya kwanza ya Sera hiyo imeshakamilika na sasa wadau mbalimbali wanatoa mapendekezo yao kuiboresha, kabla ya kupelekwa bungeni ili kutungiwa sheria.
Aidha, mikakati hiyo itakayotekelezwa ni kuhuisha muundo na utaratibu mpya wa elimu na mafunzo kwa kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa miaka mitatu na mitano anapitia elimu ya awali kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu-msingi.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alithibitisha kwa gazeti hili wiki hii mjini hapa kuhusu kukamilika kwa rasimu ya kwanza ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2013.
“Ni kweli Sera hiyo imekamilika baada ya kuandaliwa kwa miaka mitatu. Imepita kwa wadau mbalimbali, mashuleni, vyuoni na katika taasisi mbalimbali nchini ambao wametoa maoni yao. “Jumapili (kesho) tunatarajia kuwa waheshimiwa wabunge nao watapata fursa ya kuijadili na kutoa maoni yao katika semina iliyoandaliwa maalumu kwao,” alisema Mulugo katika Viwanja vya Bunge.
Alisema baada ya maoni hao ya wabunge, watapeleka Rasimu hiyo kwa mamlaka husika kwa ajili ya andiko la mwisho kabla ya kupelekwa katika Bunge lijalo ili itungwe sheria kuhusu Sera ya Elimu na Mafunzo.
Hata hivyo, semina hiyo huenda isifanyike kesho kutokana na kuingiliana na ratiba nyingine, kwani wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) watakuwa na mkutano na Mwenyekiti wao wa Taifa, Rais Jakaya Kikwete, kwenye Ukumbi wa White House mjini hapa.
Wiki moja iliyopita, wakati akiongoza kikao, Spika wa Bunge, Anne Makinda aliwaambia wabunge kuwa makabrasha waliyokuwa wakipewa na wahudumu ni kuhusu Sera ya Elimu na hivyo waende wakayasome, kwani kuna siku wataijadili.
Kwa mujibu wa rasimu, mambo mengine yanayotarajiwa kutekelezwa na Sera ni kuhuisha mitaala ya sasa ya elimu ili ikidhi muundo mpya wa elimu na mafunzo, kuhuisha sheria na taratibu mbalimbali za utoaji elimu ili ziendane na muundo mpya wa elimu-msingi.
Kuimarisha mfumo wa usimamizi, ithibati na udhibiti wa utoaji wa elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali ili kukidhi malengo na muundo mpya wa elimu-msingi.
Nyingine ni kuongeza ubora wa miundombinu katika shule za sasa za msingi ili kukidhi mahitaji na malengo ya elimu-msingi ikiwa ni pamoja na kuongeza madarasa ya elimu-msingi katika kila shule ya msingi ya sasa, kujenga maabara za sayansi na maktaba katika kila shule ya elimu-msingi.
“Kutenga rasilimali fedha za kutosha kwa ajili ya nyenzo, vifaa na zana za kufundishia na kujifunzia, vitabu vya kiada na ziada, maandiko, machapisho ya maktaba pamoja na vifaa vya maabara,” ilieleza rasimi hiyo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kuimarisha matumizi ya lugha za Kiswahili na Kiingereza katika ngazi ya elimu – msingi kama lugha za kujifunzia na kuwasiliana.
Kuweka utaratibu utakaohakikisha kuwa wanafunzi wanaomaliza elimu na mafunzo ngazi husika kwa ufanisi na wale wanaokatisha masomo au mafunzo yao kwa sababu mbalimbali, wanaendelea na kuhitimu masomo au mafunzo yao katika mfumo rasmi wa elimu na mafunzo. Jambo jingine litakalotekelezwa ni kutoa elimu kwa umma kuhusu madhumuni, malengo na matarajio ya Sera mpya ya Elimu na Mafunzo.
Rasimu ilieleza kuwa mambo chanya yanayotarajiwa kupatikana baada ya mkakati kutekelezwa ni kuwepo kwa elimu ya awali ya lazima kwa kipindi kisichopungua mwaka mmoja kabla ya kujiunga na elimu msingi, kuwepo kwa elimu msingi ya miaka 10 kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne cha sasa kwa watoto wote wenye rika la kwenda shule.
Matokeo mengine ni kuwepo kwa mfumo nyumbufu, miundo na taratibu za kujiendeleza katika mikondo anuai ya kitaalamu na kitaaluma, kuwepo kwa elimu na mafunzo yenye viwango, ubora na sifa zinazotambulika kitaifa, kikanda na kimataifa.
“Kuwepo kwa fursa mbalimbali za elimu na mafunzo zinazokidhi mahitaji ya wananchi na ya nchi kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia.
“Kuwepo kwa ugharimiaji endelevu wa elimu na mafunzo na kuwepo kwa mfumo wa elimu na mafunzo unaozingatia masuala mtambuka,” ilifafanua Rasimu ya Sera ya Elimu na Mafunzo.
Kuhusu elimu ya awali, ilieleza kuwa mkakati ni kuweka vigezo, viwango na taratibu ili elimu ya awali iwe ya lazima na itolewe katika kila shule ya elimu – msingi, na kuwa sheria, miongozo na taratibu kuhusu elimu hiyo lazima kuwekwa na kutekelezwa ifikapo mwaka 2018.
Katika elimu msingi, ni kuwa ya lazima kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, na kutolewa kwa miaka 10 na umri wa kuanza darasa la kwanza kuwa kati ya miaka minne hadi sita kulingana na uwezo wa mtoto kumudu masomo katika ngazi husika.
Shabaha katika eneo hili ni sheria na miongozo kuhusu elimu-msingi kuwekwa na kutekelezwa ifikapo mwaka 2016, mpango wa utekelezaji wa utoaji wa elimu-msingi kuwepo ifikapo mwaka 2018 na elimu-msingi kutolewa ifikapo 2018.
Kwa mujibu wa dibaji ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa, Sera mpya imeandaliwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau ikitilia maanani mafanikio yaliyoletwa na Sera zilizotangulia na kulifanya Taifa kupiga hatua katika nyanja za elimu na mafunzo.
“Sera kuu zilikuwa ni Sera ya Elimu na Mafunzo 1995, Sera ya Elimu ya Ufundi na Mafunzo 1996 na Sera ya Taifa ya Elimu ya Juu 1999 ambazo zilitekelewa sambamba na sera nyingine ambazo zinaigusa sekta ya elimu na mafunzo kama vile Sera ya Sayansi na Teknolojia 1996, Sera ya Habari na Utangazaji 2003, Sera ya Ubia kati ya Sekta ya Umma na ya Binafsi 2009 pamoja na nyingine za aina hiyo,” alisema Dk Kawambwa.