WACHEZAJI wa Bayern Munich, makocha, mabosi na mashabiki jana walioga pombe uwanjani baada ya kukabidhiwa taji lao la ubingwa wa Bundesliga.
Bayern iliandika rekodi ya kutwaa ubingwa ikiwa na mechi sita mkononi.
Miamba hiyo ya Ujerumani bado ina nafasi ya kuandika rekodi ya kutwaa “mataji matatu kwa mpigo” msimu huu wakati wakisubiri kuivaa Borussia Dortmund katika fainali ya Champions League na Stuggart katika fainali ya DFB Pokal (Kombe la Ujerumani).
Kocha anayemaliza muda wake, Jupp Heynckes na wachezaji wake waliogeshana bia – ikiwa ni utamaduni wao, baada ya ushindi wa 3-0 dhidi ya Augsburg kwenye dimba la Allianz Arena wakati walipokabidhiwa taji lao kwa kutwaa ubingwa wa Ujerumani mara ya 23.
Mtu na kocha wake
Mabao kutoka kwa Thomas Mueller, Xherdan Shaqiri na Luiz Gustavo yaliiwezesha Bayern kufunga mfululizo katika mechi 36 za Bundesliga na kuifikia rekodi yao wenyewe waliyoweka kati ya Mei 1973 na Mei 1974.
“Hakuna timu nyingine katika historia ya Bundesliga iliyocheza soka kwa namna tuliyocheza mwaka huu, mfululizo katika kiwango cha juu. Hiyo inanifanya nijivunie,” alisema Heynckes akiwa amelowa bia baada ya kuogeshwa na wachezaji wake.
Heynckes, ambaye alitimiza miaka 68 Alhamisi iliyopita, ataondoka msimu ujao kumpisha kocha wa zamani wa Barcelona, Pep Guardiola.