KUSHOTO NI ALIYEKUWA MKUU WA WILAYA YA RUNGWE MKOANI MBEYA JACKSON MSOME AKIWA NA MKUU WA CHUO CHA UALIMU TUKUYU (MSASANI) MWALIMU MATHIAS MVULA BAADA YA MAHAFALI YA 35 YA CHUO HICHO YALIYOFANYIKA MWAKA JANA.
SERIKALI imesema itaondoa changamoto zilizopo kwenye chuo cha ualimu Tukuyu (Msasani) kilichopo wilayani Rungwe mkoani Mbeya ikiwamo ya kujenga shule ya sekondari katika chuo hicho ili kuwarahisishia wanachuo kufanya mazoezi kwa vitendo.
Mkuu wa wilaya ya Rungwe, Crispine Meela. |
Kauli hiyo imetolewa na mkuu wa Wilaya ya Rungwe Chrispin Meela wakati wa mahafari ya 36 ya kuwaaga wanachuo waliohitimu kozi ya Stashahada ya Ualimu yaliyofanyika katika ukumbi wa chuo hicho.
Changamoto zilizopo chuoni hapo ni uchakavu wa majengo,mfumo mbovu wa maji katika vyoo,ubovu wa barabara yenye kilometa 3 kutoka chuoni hadi Tukuyu mjini,ukosefu wa shule ya sekondari pamoja na upungufu wa nyumba za waalimu ambapo asilimia 80 ya waalimu wanaishi kwenye nyumba zilizopo mbali na chuo.
Mkuu wa chuo hicho Mathias Mvula mbali na kuipongeza Serikali kukubali kuondoa changamoto hizo pia alitaja idadi ya wahitimu wa mwaka huu kuwa ni 491 kati ya hao wanaume ni 313 na wanawake ni 178,na kuongeza kuwa serikali inatakiwa kukitazama kwa jicho la tatu chuo hicho ambacho kinatoa waalimu wengi wa masomo ya Sayansi na sanaa kwa zaidi ya miaka sita sasa.
Aliongeza kuwa chuo hicho kinapokea wanafunzi wengi lakini majengo yaliyopo chuoni hapo ni chakavu yanatakiwa kufanyiwa ukarabati na kuwa iwapo serikali itaondoa changamoto zilizopo sifa za chuo hicho zitaongezeka na kwamba kwa sasa hali ya chuo hicho haiendani na taaluma nzuri wanayoitoa kwa kuwa majengo yaliyopo ni chakavu na yanashusha hadhi ya chuo hicho.
Alitimisha kwa kuwaasa wahitimu kuwa makini na maisha ya uraiani na kutojiingiza katika vitendo viovu,na kuwa iwapo watapangiwa kufanya kazi ya kufundisha katika shule zilizopo vijijini wasikatae kwani imekuwa ni kawaida ya waalimu kuzikataa shule za vijijini na kuzikimbilia shule zalizopo mijini na kuziacha shule za vijijini zikiwa na upungufu mkubwa wa waalimu.