Nakaaya Abraham Sumari.
KAMA kuna mtu ambaye hakujui, ngoja nikusaidie kujitambulisha kwake. Unaitwa Nakaaya Abraham Sumari. Ulizaliwa Septemba 3, 1982 jijini Arusha, Tanzania. Wewe ni icon mkubwa wa R&B na Hip hop Bongo. Unakumbuka Mr. Politician? Ndiyo ngoma iliyokupa mashavu, ukawika.
Kama bado hawajakufahamu au wamesahau, naendelea. Wewe ni dada mkubwa katika familia ya watoto watano kwa Mzee Abraham Sumari. Mdogo wako ni Nancy Abraham Sumari. Miss Tanzania na Miss World Afrika mwaka 2005.
Kwa mara ya kwanza ulionekana kwenye shoo ya kwanza Afrika Mashariki ya Tusker Project Fame iliyoruka Oktoba Mosi hadi Desemba 17, 2006.
Baada ya shindano hilo ulirejea Bongo kwa ajili ya kufanya muziki rasmi.
Singo zako za Malaika na Mr Politicia zilifanya poa sana redioni, Afrika Mashariki. Ukawa maarufu kila kona Bongo. Nani anabisha?
Haikuishia hapo, bidada ulisaini mkataba na kampuni kubwa ya muziki duniani ya Sony BMG mwaka 2009 wakati wa ziara zako za kimuziki nchini Denmark.
Pia uliteuliwa kuwania na kupata tuzo mbalimbali zikiwemo zile za Kisima na Pearl of Africa. Si jambo dogo. Utambulisho mrefu unaishia hapa.
Wiki iliyopita ulizindua ngoma yako mpya, Utu Uzima Dawa. Wakati ukitambulisha wimbo huo Radio Clouds, ulizungumza vitu viwili au vitatu.
Kwanza pole kwa ajali uliyopata Mbauda, Arusha ukakaa kitandani mwaka mzima. Pili hongera kwa kuwa na ujauzito wa miezi kadhaa, japo hukututajia shemeji yetu.
Pia uliwaomba radhi Watanzania na wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kurudisha kadi ya chama hicho na kuchukua ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2010.
Uliwaomba Watanzania wajue kuwa wewe ni binadamu na unafanya makosa na hawawezi kujua ni kwa namna gani unateseka sana moyoni kwa hali hiyo.
Ni kweli hujawahi kulizungumzia suala hilo lakini unajuta sana moyoni.
Ulikiri pia kwamba kufanya hivyo ulibugi ramani na si kweli kwamba ulipewa fedha na kufanya usaliti.
Ulikubali kwa kinywa chako kwamba uliingia kwenye siasa kwa sababu ya ushawishi wa watu kisa wimbo ulioutoa wakati huo wa Mr Politician.
Baada ya kuingia kwenye siasa na kuhamia chama tawala na kuambulia patupu ndipo ukagundua kumbe siasa ni mchezo mchafu. Ukakata tamaa na sasa upo njia panda.
Nakupa pole lakini iwe fundisho kwa wasanii wengine ambao hutumika kisiasa kwa ahadi kemkemu lakini baada ya kutumiwa hutupwa wakafie mbali. Wapo wasanii wengi wa Bongo Fleva tumewashuhudia wakizunguka kuwafanyia kampeni wanasiasa ili washibishe matumbo yao. Nakaaya alifanya hivyo, watu wa Arusha wanalijua hilo.
Nakubaliana na Nakaaya kuwa hakuna binadamu ambaye huwa hakosei lakini kisiwe kigezo cha kuwakatisha wengine tamaa. Yupo Rapa Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ mjengoni. Wapo wengine wanaojipanga kugombea 2015 wakiwemo Mrisho Mpoto, Jacob Steven ‘JB’ na wengine wengi. Jipangeni na wala msikate tamaa kwa kumwangalia Nakaaya.
Mbona wapo wabunge wengi tu mjengoni hawana hoja zaidi ya matusi? For the love of game!
Chanzo:globalpublishers info